SIKU YA AFYA YA AKILI DUNIANI.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Lukiza Autism Foundation na muandaaji wa mbio ya Run 4 Autism Tanzania; inayojihusisha na kutetea watu wenye hali ya Usonji/Autism; amewataka wazazi wenye watoto wenye Usonji kutokata tamaa na kuwalea watoto wao kwa upendo, pamoja na changamoto zote wanazozipitia katika ulezi.
Akizungumza katika Kongamano la kwanza la Kitaifa la afya ya akili nchini lililofanyika katika ukumbi wa mwalimu Julius Kambarage Nyerere ( JINCC ), mkurugenzi huyo ameiomba Wizara ya afya kutatua changamoto zinazowakabili wazazi wa watoto hawa, kama vile gharama kubwa za mazoezi tiba, uchache wa wataalam wa utambuzi wa hali ya Usonji na wataalam wa mazoezi tiba, uchache wa vituo vya afya vinavyotoa huduma za mazoezi tiba na shule au vituo jumuishi au maalum.
Akipokea tuzo ya ubalozi wa afya ya akili kutoka kwa Waziri wa afya, Mhe Ummy Mwalimu, kutokana na mchango wake katika kuelimisha jamii juu ya afya ya akili hususan Usonji, bi Hilda Nkabe alimshukuru Mhe. Ummy mwalimu na Wizara ya afya kwa ujumla kutambua mchango wake kwenye sekta hii na kwa kufanikisha uwepo wa Kongamano hili la kwanza la kitaifa la afya ya akili na kufungua mazungumzo mapana ya Kitaifa kuhusu afya ya akili nchini Tanzania.
Comments
Post a Comment