SPIKA WA BUNGE LA KWALE AKANUSHA MADAI YA UTEPETEVU.
bunge la kaunti ya Kwale.
Habari:Caroline Katana.
Spika wa bunge la kwale Seth Mwatela Kamanza ametetea afisi yake dhidi ya madai kuwa amewaeka bungeni wajumbe wateule watano kinyume cha sheria ,akiyataja madai hayo kuwa yenye kupotosha na kudhalilisha afisi yake kwani watano hao wamo bungeni kufuatia agizo la mahakama.
Kesi dhidi ya wajumbe hao wateule iliwasilishwa mahakamani na aliyekuwa mjumbe mteule Mary Kalinga ,kwa kile alichokitaja kuwa uteuzi wao ulifanywa kwa njia isiyokuwa halali.
Kamanza akiafiki kufahamu kesi inayowakabili wajumbe hao japo kusema kuwa hana mamlaka ya kuwatoa bungeni baada ya mahakama kuu kutoa agizo la kuendeleza majukumu bungeni humo hadi pale kesi dhidi yao itakapotolewa uamuzi .
Amehoji kuwa baada ya mahakama kuu kutoa agizo la kusimamishwa kwao mnamo tarehe 14 mwezi September mwaka jana ,watano hao walitafuta haki katika mahakama ya upeo kabla ya kesi hio kurudishwa katika mahakama kuu ambayo ili waamuru kurudi bungeni kwa mara nyingine.
“ Afisi yangu inatekeleza shughuli zake kwa mjibu wa sheria za kikatiba ,na mimi kama spika na wakili ni sharti ni hakikishe kila sheria inafuatwa ili kila haki ya mkaazi inalindwe ,”Asema spika Kamanza.
Akigusia swala la bunge hilo kukosa nguvu katika utekelezaji wa majukum yake baada ya kutekwa na upande wa afisi ya gavana wa Kwale Fatuma Achani ,spika amesema hizo ni porojo tu.
Kamanza ameyataja madai hayo kukosa msingi kwani kwa kipindi cha miaka miwili, bunge hilo limeweza kupitisha sheria Zaidi ya sita zinazofaa kutekelezwa ili zimfaidi mkaazi.
“ Sisi kama bunge tuna wahakikishia wakaazi wa Kwale kuwa tunatekeleza majukumu yetu ya uwakilishi ,utungaji sheria na ufuatilizi wa utendakazi wa upande wa afisi ya gavana ,tumepitisha sheria Zaidi ya sita na zengine zinashughulikiwa ,”Ahoji spika Kamanza.
Kadhalka ameafiki bunge hilo kuendeleza mchakato wa kuwahoji mawaziri dhidi ya tetesi ibuka za utepetevu katika wizara zao hatua inayowapelekea wakaazi kukosa huduma hususan ni zile za afya .
“ Sio eti bunge limetepetea katika utendakazi wake ,tumeweza kuwaita mawaziri mbele ya bunge kutuelezea jinsi wanavyoendesha majukumu yao, hivi majuzi kumekuwa na lalama kutoka kwa wakaazi kuhusu ukosefu wa vifaa muhimu katika hospitali ya Kwale na ile ya Kinango na tayari tushamfikisha waziri wa afya Francis Gwama bungeni atueleze sababu zinazopelekea hali duni za afya katika hospitali hizo ,”Asema spika Kamanza.
Aidha amesema kuwa tayari ripoti ya uchunguzi dhidi ya lalama za utendakazi wa wizara ya afya imewasilishwa bungeni na itatoa mwongozo wa hatua zitakazochukuliwa katika wizara hio ya afya .
Wakati uohuo amedokeza kuwa changamoto ya ukosefu wa fedha kutoka kwa hazina ya kitaifa kuwa changamoto kuu inayodumaza utendakazi wao .
“Katika mwaka wakifedha uliopita tumekuwa na changamoto ya kupata fedha kutoka kwa hazina ya fedha ya kitaifa haswa ni zile za kusimamia shughuli mbalimbali za afisi ,kufikia mwezi June tulikuwa tunaelekea karibu miezi saba bila pesa zozote za kusimamia shughuli mbalimbali za kaunti nzima ,hatua iliyotulazimu kutumia pesa za mifuko yetu sisi wenyewe ,”Asema spika Kamanza.
Hata hivyo ameafiki mabunge ya humu nchini pamoja na baraza la magavana wanaendeleza mazungumzo na serikali kuu ili kuona kuwa mgao wa fedha katika magatuzi unawafikia kwa wakati.
Spika Kamanza akiwataka wakaazi wa Kwale kufuatilia utendakazi wa bunge hilo katika mitandao ya kijamii ili wafahamu shughuli zinazoendelea bungeni.
“ Kazi zetu nyingi zinafanywa na kamati za bunge ,na kamati hizi hukutana kila wiki kuanzia siku ya juma tatu ,jumanne ,jumatano na hadi jumamosi ,ningewaomba wananchi wa Kwale wafuatilia vikao hivi na wawe na subra mana kila kazi iko na changamoto zake ,na baadhi ya hizi changamoto ni ukosefu wa fedha na uchunguzi katika wizara mbalimbali ,”Asema spika Kamanza.
Kiongozi huyo amekanusha kuwepo na mgawanyiko bungeni humo ,akisema kwamba wameungana ili kufanikisha majukumu yao kwa wananchi kwa mjibu wa katiba.
Kauli ya spika Kamanza imeungwa mkono na mwakilishi wa wadi ya Mwereni Manza Beja huku akipuzilia mbali madai kuwa wajumbe na spika wa bunge hilo wamekuwa wakitalii mataifa ya nje badala ya kufanikisha shughuli za bunge.
“ Mheshimiwa yeyote kusafiri nchi za nje ni lazima apate kibali kutoka kwa wizara ya ugatuzi , ukipatikana taifa la nje bila idhini hio ni kinyume cha sheria ,ni sharti mtu awe na malengo muhimu ya safari hizo ,si kweli kwamba spika na baadhi ya wajumbe wamekuwa wakitalii katika mataifa ya kigeni ,”Akiri bw.Beja .
Hata hivyo ameshikilia kuwa bunge linatekeleza shughuli zake kwa mjibu wa sheria pasi na vishawishi kutoka afisi ya gavana.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wateule wanaohudumu bungeni kupitia agizo la mahakama Josphine Kinyanjua ameshikilia kuwa watano hao waliteuliwa kihalali ili kuwakilisha makabila madogo kaunti ya Kwale kwa mjibu wa sheria ya katiba.
Josphine akisema kuwa wamo bungeni kufuatia agizo la mahakama kuu wala sio kinyume cha sheria hivyo wako na haki yakutekeleza majukumu bungeni kama wawakilishi wengine hivyo kutaka swala hilo kutotiliwa siasa za ukabila hadi pale mahakama itakapotoa uamuzi wa mwisho dhidi ya kesi hio.
Haya yanajiri siku chache baada ya kiongozi wa chama cha Uzalendo Richard Onsongo kumtaka spika Seth Mwatela Kamanza kuwatimua bungeni wawakilishi hao wateule na kuwataka kurudisha mishahara na marupurupu ya miezi miwili waliyopokea kwa madai kuwa hawamo bungeni kisheria kwani walichaguliwa kwa njia isiyokuwa halali .
Onsongo akiitaka tume huru ya uchaguzi na mipaka kuhakikisha uteuzi wa wajumbe wateule Kwale unawafaidi wenyeji na ujumuishe jamii ya watu wanaoishi na uwezo maalum.
Comments
Post a Comment