RIPOTI YA UTAFITI WA ELIMU ENEO LA PWANI YAZINDULIWA RASMI NA SHIRIKA LISILOKUWA LA KISERIKALI LA USAWA AGENDA.
Taarifa yake : Caroline Katana.
Shirika lisilokuwa la kiserikali la Usawa Agenda kwa ushirikiano na mashirika mbalimbali ya kijamii
ukunda wa pwani yamezindua ripoti maalum inayofahamika kama Foundation Literacy and Numeracy
Assessment FLANA yenye tathmini ya viwango vya elimu eneo la pwani.
Hii baada ya utafiti uliofanywa katika kaunti zote 47 nchini mwaka uliopita ili kutathmini viwango vya
kusoma ,kuandika na kuhesabu miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka kati ya 6 -16 ili kuchochea sera zenye ushahidi ambazo zingeweza kusababisha ujifunzaji sawa kwa watoto wote.
Mratibu wa shirika la Usawa Agenda kaunti ya Kwale ambaye pia ni mwanachama wa shirika la
kijamii la Kwale Youth and Governance Consortium KYGC Amani Lugogo amesema kuwa utafiti huo
ulijumuisha vijiji 230 ,nyumba 6,348 , watoto 3,016 na shule 226 ukunda wa pwani.
“ Leo hii tuko hapa kuzindua ripoti ya elimu ya pwani ambapo kaunti zote sita zimejumuishwa ,tulifanya
zoezi hili la utafiti Kenya nzima mwaka jana na tukazindua ripoti ya kitaifa ,na malengo haswa ni kuona kwamba changamoto sugu zilizozingira swala zima la elimu zinatatuliwa ,ndio maana tumehusisha washikadau kutoka idara ya elimu ,viongozi wa kisiasa ,viongozi wakidini ,wazazi na wazee wa mitaa, tunataka kuona ni vipi tunaeza zungumziana ili kuboresha elimu eneo la pwani ,”Asema bw.Lugogo
Gabriel Nyiro mwakilishi wa shirika la Usawa Agenda kaunti ya kilifi.
Gabriel Nyiro mwakilishi wa shirika hilo la Usawa Agenda kaunti ya Kilifi ambae pia ni mwanachama wa shirika la Mission for Community and Initiative Development ameafiki kuwepo na changamoto ya wanafunzi kutofahamu kusoma hata vitabu vya madarasa waliyosoma awali.
“ Mara nyingi tumepata mwanafunzi wa darasa la 4 haezi kutatua hesabu ya darasa la 2 na mwanafunzi wa darasa la 8 hawezi kusoma kitabu cha darasa la 6 , ndio maana twajiuliza hawa wanafunzi wako shuleni kusoma ama wamo shuleni kwa sababu shule ni lazima ziwe na wanafunzi ,haya ni maswala ambayo tumekuwa tukijiuliza kila mwaka tunapofanya utafiti ,”Asema bw Nyiro.
Faraj Mohamed wa shirika la Uwezo Youth Group kaunti ya Lamu amedokeza kuwa utafiti huo ulioanza mwaka 2009 umeonyesha kuwa idadi kubwa ya watoto wakiume Lamu wamesusia masomo ikilinganishwa na watoto wakike.
“Kimtazamo wangu kaunti ya Lamu bado viwango vya elimu viko chini ,kulingana na hii ripoti wasichana wengi ndio wanapenda masomo kushinda wavulana ,watoto wakiume hujihusisha sana na maswala ya baharini masomo inakuwa kwao sio muhimu ,”Asema bw Mohamed .
Bw Mohamed akitoa changamoto kwa washikadau wa elimu kushirikiana na kutathmini na kutoa suluhu kwa changamoto zinazokabili swala la elimu Lamu na pwani nzima kwa ujumla .
“Nimefanyakazi na mashirika mbalimbali ya elimu na swala linalojitokeza ni wazazi na walimu kukosa kulipa swala la elimu kipao mbele kaunti ya Lamu , kwa hio endapo wadau wote wa elimu wataingilia kati tatizo hilo basi huenda viwango vya elimu vika imarika ,”Asema bw.Mohamed
Patrick Mwadime mratibu wa shirika la Usawa Agenda kaunti ya Mombasa amethibitisha asilimia 91.7 ya watoto wa shule za msingi kaunti hio ya Mombasa kuhudhuria masomo huku asilimia 8 hawajulikani waliko .
“Tunajiuliza hii asilimia 8 ya watoto wako wapi na kwa nini hawaendi shule kwa sababu elimu ni haki ya kimsingi kwa kila mtoto , changamoto zipo na ni sharti zipate suluhu ,tulidhania ripoti ikitoka tutapata asilimia 100 ama 99.9 ya watoto wako shule hapa Mombasa lakini bado kuna wale ambao bado wako nje ,ripoti hii haiangazii elimu tu, ila elimu bora ,”Asema bw.Mwadime.
Kaunti ya Taita taveta ni miongoni mwa kaunti zilizo na viwango vya chini vya elimu licha ya serikali na mashirika kutia juhudi za kuboresha elimu katika kaunti hio.
Mimba za utotoni na utimizi wa mihadarati ikitajwa kuwa changamoto sugu inayolemaza elimu kaunti ya Taita taveta ,”Asema Dishon Mbagau ,mwakilishi wa shirika la Uwasa Agenda Taita taveta.
Comments
Post a Comment