UFISADI KATIKA SERIKALI ZA KAUNTI UMESAMBARATISHA HUDUMA ZA MAJI KWA WANANCHI
Taarifa yake : Caroline Katana
Afya bora ,maji safi na salama ni mahitaji msingi ya binadamu ,lakini pia yana umuhimu wake kwa viumbe wote wanaoishi duniani.
Walimwengu wanapaswa kufaidika na haki hii msingi katika maisha yao .
Uhaba wa maji safi na salama unaweza kuwa chanzo cha migogoro kinzani kwa siku za usoni ikiwa kama serikali ya kitaifa na zile za kaunti hazitasimama kidete kulinda vyanzo vya maji pamoja na kutambua kwamba maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu.
Huduma bora za maji safi na salama ni kichocheo kikuu cha maisha na afya bora Zaidi.
Dhana ya maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu ni agenda iliyoibuliwa hivi karibuni ,lakini inaendelea kushika kasi kubwa sana katika jumuiya ya kimataifa kutokana na unyetiwake.
Ndio maana kuna haja ya kuwa na miundo mbinu ya kisheria ,kiufundi ,kijamii na kisiasa ili kuanzisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa utunzaji bora wa vyanzo vya maji.
Maji ni muhimu sana kwa ustawi ,maendeleo na mafao ya wengi.
Kenya imeorodheshwa miongoni mwa nchi zenye uhaba wa maji duniani ,hali hii inatokana na mizunguko ya mara kwa mara ya hali ya hewa kali inayoharibu mali asili.
Takriban asilimia 60 ya wakenya wanapata maji salama ya kunywa ,asilimia 29 wanapata
huduma msingi za vyoo.
Nchini kenya watu milioni 9.9 hunywa maji moja kwa moja kutoka kwa vyanzo vya maji vilivyochafuliwa na inakisiawa kuwa watu milioni tano hawana vyoo na wanafanya haja kubwa wazi.
Asilimia 25 pekee ya watu nchini Kenya wako na vifaa vya kunawia mikono , sabuni na maji nyumbani mwao.
Ukosefu wa usalama wa maji pamoja na ukosefu wa bidhaa na huduma za usafi wa mazingira,unaweka afya ya umma hatarini , inadhoofisha ukuaji wa uchumi ,ukosefu wa utulivu wa kisiasa na huchangia ukosefu wa usawa.
Katiba ya Kenya chini ya kifungu cha 43 (1)(d) inamhakikishia kila mtu nchini Kenya haki ya kupata maji safi na salama kwa wingi wa kutosha.
Ingawa maji ni rasilimali ya kitaifa na inashirikishwa katika kaunti zote ,huduma za maji ziligatuliwa.
Serikali za kaunti nchini Kenya hazijatoa ripoti kuhusu miradi ya maji inayotekeleza katika kaunti zao.
Tangu kuanza kwa ugatuzi mwaka 2013 ,serikali za kaunti hazijawasilisha Data ya pamoja na ya kina iliyoandaliwa kuhusu hali ya utimilifu wa wajibu wao ,ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma katika kaunti zote ,mapengo yaliyopo na mikakati yakuziba mapengo hayo.
Kuna ukosefu wa uwajibikaji katika utoaji wa huduma za maji katika maeneo ya mashinani ambayo yanachangia sehemu kubwa ya upatikanaji wa maji nchini.
Muungano wa mashirika ya kutetea haki ya maji na usafi nchini KEWASNET ukielezea wasiwasi wao juu ya viwango duni vya uwajibikaji juu ya jukumu la kikatiba la huduma za maji na usafi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali nchini Kenya.
Katika mkao wa siku mbili wa majadiliano juu ya uwajibikaji wa serikali za kaunti kuhusiana na
huduma za maji ulifanyika Diani kaunti ya Kwale ,mkurugenzi mkuu wa mashirika ya kijamii ya kutetea haki ya maji nchini wa Kenya Water and Sanitation Malesi Shivaji akisema kuwa ni sharti uwajibikaji wa maji na usafi wa mazingira nchini Kenya uimarishwe.
“Kushindwa kwa uwajibikaji kunaiacha jamii na ukosefu wa ufahamu wa wazi na utaratibu wa kutatua malalamiko dhidi ya serikali kushindwa kutimiza haki zao za maji na usafi wa mazingira ,” Asema bw.Shivaji.
Kulingana na ripoti ya taasisi ya Kenya ya utafiti na uchambuzi wa sera za umma (KIPPRA ) kaunti nyingi zinakabiliwa na vikwazo vya uwezo ,ikiwa ni pamoja na utaalam wa kiufundi wa kutosha na rasilimali duni za usimamizi na uangalizi bora wa kifedha.
Aidha bw.Shivaji amesema kwamba wakati mifumo ya kisheria iko ,kuna migogoro mikubwa ambayo baadaye inazuia utekelezaji mzuri wa uwajibikaji.
“Kwa kushindwa kutoa maelezo ya wajibu ulioidhinishwa na katiba kunasababisha ukosefu wa uelewa juu ya maeneo ambayo yanahitaji maboresho au msaada ambao unaweza kutolewa nawashirika ,” Asema bw.Shivaji.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la CESPAD Ashah Shaaban ameelezea masikitiko yake ya wananchi kupata huduma duni za maji hivyo akiitaka serikali ya kitaifa na zile za kaunti kubuni utaratibu wa kutoa Data ya wakati halisi ya sekta ya maji ambayo inapatikana kwa umma na ambayo inaweza kutumika kufanya maamuzi kwa wakati ufaao.
Kadhalka akizitaka serikali za kaunti zitekeleze kikamilifu mamlaka yao ya kuhifadhi udongo na maji ,kaunti zifuate miongozo ya ushiriki wa umma ili kuongoza utendakazi wake pamoja na kuchukua jukumu kuu katika uratibu wa washirika na shughuli za sekta tofauti kubwa na sektandogo.
Bi .Shaban aidha akizitaka serikali za kaunti kutekeleza kikamilifu mwongozo wa utoaji wa huduma za maji vijijini kama ulivyoratibiwa na bodi ya uthibiti wa huduma za maji nchini WASREB.
Akigusia swala la ufisadi ,mkurugenzi wa shirika la Kenya Water For Health Organization KWAHO ,Patrick alubbe amehoji kuwa ufisadi katika sekta ya maji kuwa chanzo cha wakenya kukosa maji salama.
“ Hatuwezi kusema kuwa hakuna ufisadi , kama unastahili unisambazie maji na umefeli huo tayari ni ufisadi ,kuna mengi ambayo yanaendelea katika hio sekta ya maji ambayo yanahitaji kurekebishwa ,kitu tumeona ni kwamba pesa zile za maji zinazokuja kwa kaunti mara nyingi huwa ni pesa za kutosha ila zinapofika katika mabunge ya kaunti kila mwakilishi wadi anataka apewe pesa kidogo , kwa hio tunataka kaunti zieke kipao mbele miradi ya maji inayopania kutekeleza badala ya kueka miradi ya maji kila sehemu yenye gharama za juu ambayo wakaazi hushindwa na kuitunza hivyo kukosa kufaidika ,”Asema bw. Alubbe.
Tangu kuanza kwa serikali za ugatuzi sekta ya maji ni kati ya wizara kuu zinazotengewa mgao mkubwa wa fedha katika kila mwaka wakifedha na serikali za ugatuzi ,kinaya ikiwa asilimia kubwa ya wakaazi wanaendelea kukumbwa na uhaba mkubwa wa maji ,baadhi wakilazimika kununua bidhaa hio kwa bei za juu mno huku walala hoi wakisalia kutumia maji ya mto na visima ambayo sio salama.
Mfano hai ukiwa wa wakaazi wa kijiji cha Nyando ,Matuga kaunti ya Kwale kusalia kuhangaikia bidhaa hio muhimu baada ya kushindwa kusafisha matope yaliyozagaa kwenye kisima walichochimbiwa na serikali ya kaunti ya Kwale kufuatia hali zao za uchochole.

.png)

Comments
Post a Comment