FUO YA BAHARI YA DIANI YANG’AA KWA MARA YA NANE AFRIKA.
Taarifa yake : Caroline Katana.
Taifa la Kenya linakila sababu ya kusherehekea baada ya fuo ya bahari ya Diani kutambulika tena kama eneo la fukwe bora Zaidi linaloongoza barani Afrika katika tuzo za dunia za tuzo za afrika za 2024 ( World Travel Awards ,Africa Gala Ceremony 2024) iliyofanyika katika ukumbi wa sherehe wa Diamonds Leisure Beach and Golf Resort, Diani , Kenya.
Hii ikiwa ni mara ya nane kwa fukwe hio ya Diani kutambulika kwa ubora wake ,hivyo kuimarisha mvuto wake kwa wageni wakimataifa na wa ndani.
Hafla hio imewaleta pamoja viongozi na wabunifu kutoka bara zima la Afrika ,mashirika ya usafiri yaliyoweka viwango vipya vya ubora na uvumbuzi katika sekta hio ya utalii.
Gavana wa Kwale Fatuma Achani aliyehudhuria sherehe hio amesema kuwa ushindi wa fukwe hio, baadhi ya hoteli za kitalii na uwanja wa ndege wa Ukunda kusini mwa pwani umechochewa na ushirikiano bora kati ya serikali kuu ,ile ya kaunti na waekezaji katika sekta ya utalii.
“Tumehakikisha fukwe yetu inasalia kuwa safi pamoja na kuimarisha usalama wa wageni na wenyeji wanaozuru fuo hiii ya Diani , tumeeka taa za barabarani ,tumefungua barabara zinazoshuka fuoni ,na kwa sasa hivi kupanuka kwa uwanja wa ndege wa Ukunda na ufunguzi wa barabara ya Dongo-kundu kumechangia pakubwa kuimarika kwa utalii kusini mwa pwani ,”Asema gavana Achani.
Aidha amedokeza kuwa hatua hio ni ishara tosha kuwa kaunti ya kwale sasa imefunguka katika maswala ya uekezaji na biashara mbali na utalii.
Kadhalka kiongozi huyo akihoji kuwa ataendelea kuboresha miji ya kaunti hio ili kuhakikisha maendeleo endelevu kwa wananchi wake.
“ Miji yetu sasa iko katika kiwango cha manuspaa ,Kwale ,Kinango na Diani na Lungalunga ,katika ile mipangilio yetu yakifedha tutahakikisha kuwa tunaendelea kudumisha usafi na uboreshaji wa miji hio ili kuzidi kufungua nafasi za uekezaji na kibiashara ,”Asema gavana Achani .
Gavana Achani aidha akisema kuwa kutambulika kwa fuo ya Diani ,hoteli za kitalii na uwanja wa ndege wa Ukunda, barani Afrika ni ishara ya kuwavutia watalii wengi Zaidi wa ndani na wale wa nje hivyo kufungua nafasi za ajira kwa vijana pamoja na kuimarisha ushuru wa kaunti hii.
Rais wa planhotel hospitality group Sara Rosso –Cipolini amesema kuwa sherehe hio ina umuhimu mkubwa katika sekta ya utalii kote ulimwenguni .
Aidha ameeleza kuwa sekta hio ya ukarimu ( hospitality ) kwa takriban miaka kumi na tano imekuwa ikipata hadi tuzo Arobaini na tano kila mwaka hatua ambayo imekuwa ya faida kubwa katika sekta ya utalii.
Meneja mkuu wa hoteli ya Diamonds leisure beach and golf resort Andrew Cook ameelezea fahari yake ya kuandaa hafla hio ya kifahari ,akisema kuwa ni sherehe muhimu kwa hoteli hio na sekta ya ukarimu inayokua nchini Kenya.
Bw. Cook akielezea kufurahishwa kwake kwa hoteli hio kuwa miongoni mwa hoteli za kitalii zilizotambulika kwa ubora wake barani Afrika.
Angama Amboseli ,nyumba ya kulala wageni yenye hema nzuri iliyo katika eneo la Kimana Sanctuary nchini Kenya ilitmbulika kama hoteli mpya inayoongoza Afrika.
Meneja wa hoteli ya kitalii Leopard beach resort and spa katika kitengo cha makazi Joan Ndung’u hakuficha tabasamu lake baada hoteli hio kupata tuzo kwa mara ya tatu mfululizo .
“Tulituzwa mwaka 2022 /23 na mwaka huu wa 2024 pia tumetuzwa kwa mara nyingine kwa kuwa African leading beach resort na hii ina umuhimu mkubwa sana kwetu na wageni wanaozuru hoteli yetu ,”Asema bi .Ndung’u.
Bi.Ndung’u akisema kwamba tuzo hio imewapa changamoto ya kuendelea kuboresha bidhaa zao ili kuhakikisha mahitaji ya wageni yanaafikiwa kikamilifu .
Kadhalka ameipongeza serikali ya kaunti ya Kwale kwa kuwapa nafasi nzuri ya kufanikisha shughuli zao za kitalii hatua ambayo imepelekea wenyeji kupata nafasi za ajira pamoja na kuimarika kwa biashara eneo la Diani .
Mji mkuu wa Nairobi ulitunukiwa maeneo yanayoongoza kwa kusafiri kibiashara Afrika huku klabu ya safari ya kifahari ya Fairmont mountain Kenya ilipata sifa ya African’s leading hotel ,Somerset Westview mjini Nairobi ikitunukiwa kama ghorofa zinazoongoza Afrika .
Katika sekta ya usafiri wa anga ,shirika la ndege la Kenya Airways lilipaa sana na kutwaa tuzo za Africa’s leading Airline na Africa’s leading airline-business class ,uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta wa Nairobi ulizidisha sifa za usafiri wa anga kwa kupigiwa kura ya uwanja wa ndege unaoongoza Afrika .
Mji wa pwani wa Durban uliendelea kupaa kama kivutio cha juu cha biashara ,na kupata jina la mikutano inayoongoza Afrika ,wakati huo huo bandari ya Cape Town ilitambulika kama bandari ya kuongoza kwa safari za baharini barani Afrika ,ushuhuda wakuongezeka kwa umuhimu wake katika sekta ya bahari na utalii .
Tanzania illibuka mshindi kwa kutwaa mataji mengi ya kifahari ,taifa hilo lilitawazwa kama Africa’s leading destination ,huku bodi ya utalii Tanzania ikipokea heshima ya bodi ya utalii inayoongoza Afrika .
Miongoni mwa hazina za asili za Tanzania hifadhi ya taifa ya Serengeti ilipewa jina la hifadhi ya kitaifa inayoongoza Afrika na mlima Kilimanjaro ulipata tuzo ya kivutio kinachoongoza kwa watalii Afrika na hivyo kuimarisha sifa ya Tanzania kama kivutio cha lazima cha kutembelewa na wapenda matukio (adventure) na wapenzi wa asili sawa.
Sherehe za tuzo za dunia za tuzo za Afrika za 2024 zilikuwa sherehe bora za utalii barani Afrika huku washindi kutoka kanda zote wakionyesha ubora Zaidi ambao bara linapaswa kutoa huku viongozi wakiendelea kuvuka mipaka ya ukarimu na usafiri ,hadhi ya Afrika kama kivutio kikuu cha utalii inatarajiwa kufikia kilele kikubwa Zaidi .
Comments
Post a Comment