IDADI YA REFARII /WAAMUZI WAKIKE WANAOFUZU KILA MWAKA YAONGEZEKA KWALE.
Taarifa yake : Caroline Katana
Katika soka refarii anakuwa na nafasi kubwa sana ya kuufanya mchezo wa soka kuwa mzuri au kuuharibu.
Katika soka refarii anakuwa na kazi ya kusimamia sheria za mchezo wa soka na kama muamuzi wa mwisho katika mechi , refarii ndio ana uwezo wa kuamuru pambano liendelee au lisiendelee.
Jumapili iliyopita waamuzi wa kike wanane kati ya waamuzi 26 walifuzu kuchezesha timu mbalimbali za soka kaunti ya Kwale na hata ligi za taifa.
Mafunzo hayo yalitolewa na shirika la Sambasports Youth Agenda kwa ushirikiano na usimamizi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Basetitanium na shirikisho la soka la FKF tawi la Kwale.
Idadi ya waamuzi wa kike inaongezeka pia ,mwaka wa 2013 refarii wakike watano walifuzu kati ya refarii ishirini na nne waliopokea mafunzo hayo.
Ubaguzi wa kijinsia kutoka kwa wachezaji na watazamaji ,ukosefu wa kuajiriwa kwa wanawake katika fani hio na vyombo vya soka ,dhana hasi za watazamaji ni baadhi ya vikwazo vinavyowakabili wanawake katika kusimamia mechi za soka na michezo mingine kwani hutunga mazingira ya uhasama kwa taaluma hii.
“Tumekuwa tukijifunza kwa bidii sana kwa sababu wengine husema wanawake hawawezi kukimbia kwa kasi ya wanaume ndio maana hatuwezi kuwa wanaume ,lakini tunaweza kufanya tuwezavyo kuwa katika kiwango sawa ,” Asema bi Ndizi.
Bi .Ndizi akisema kuwa ndoto yake ni kujiunga na waamuzi wakike duniani na kuchezesha mechi za kimataifa ,akiitaja hatua hio kuondoa dhana potofu dhidi ya mtoto wakike katika Nyanja ya soka.
“ Hakuna kitu ambacho hakiwezekani ,niling’ang’ana sana kati ya wanaume saba na nikaibuka kuwa muamuzi wa katikati ,akinadada wasiogope kujiunga katika Nyanja hii ya soka wajitokeze na wakuze talanta zao ,” Asema bi .Ndizi.
Omar Abdallah kimwaga mwakilishi wa London FC aliyeshiriki katika mafunzo hayo ya refarii ametaja mafunzo hayo kumuwezesha kuzifahamu sheria kumi na saba za soka .
“Mimi kama refarii wa katikati nimezielewa Zaidi sheria za mchezo wa soka na nina uwezo wakuwafunza hata mashabiki walio na tabia za kuwakosoa refarii kwa kukosa kuzifahamu sheria ,”Asema bw Kimwaga.
Hata hivyo refarii Kimwaga amedokeza kuwa yuko tayari kukabiliana na changamoto za aina yeyote katika mchezo huo wa soka.
Mwenyekiti wa shirikisho la FKF kaunti ya Kwale Hamisi Mwakoja amehoji kuwa katika soka ya kiulimwengu malengo ya FIFA ni kuona kuwa kuna timu za akinadada na zile za wanaume zinacheza ligi sawa kufikia mwaka 2032.
Hata hivyo ameafiki kuwa dhana potofu za mashambulizi mabaya ya refarii na masaa ya kucheza soka kuwa kikwazo cha akinadada wengi kujiunga na fani ya urefarii .
“Kuna hofu kuwa mwanadada akiwa refarii anaweza kushambuliwa wakati wowote ,na hii imekuwa changamoto kwetu sisi kuwapata akinadada wengi ,”Asema bw.Mwakoja .
Kadhalka amehoji kuwa kaunti ya Kwale hadi sasa iko na refarii 268 miongoni mwao wakiwa akinadada.
Kiongozi huyo wa FKF akilitaja shirika la Sambasports Youth Agenda na usimamizi wa kampuni ya base titanium kuchangia pakubwa ukuaji wa soka katika kaunti ya Kwale.
Mkurugenzi wa shirika la Sambasports Youth Agenda Mohamed Mwachausa akisema kwamba malengo makuu ya shirika hilo ni kukuza talanta na kudhibiti tabia potofu miongoni mwa vijana kupitia mafunzo ya urefarii na makocha.
“ Hii ni awamu ya pili ya kufundisha refarii kaunti ya Kwale kupitia ushirikiano wa FKF na ufadhili wa basetitanium ,mwaka jana mwezi wa kumi tulifundisha refarii ishirini na wane na watano walikuwa akinadada ,tulipanga kuwafundisha akinadada Zaidi ya kumi lakini haikuwa rahisi kuwapata ,mwaka huu imekuwa rahisi kuwapata kwa sababu walipata motisha ya wale refarii wakike tuliowafundisha mwaka jana kutokana na sifa za kazi nzuri wanayofanya uwanjani pamoja weledi wao katika fani hio ,tuna Imani mwakani tunaweza kupata wasichana Zaidi katika fani hii ya urefarii na ukufunzi ,”Asema bw.Mohamed.
Bw.Mwachausa kadhalka amewata refarii hao na wachezaji kwa ujumla kudumisha nidhamu ,akisema kuwa talanta bila nidhamu hulipa hasara badala ya faida.
Bw.Mwachausa aliyekuwa akizungumza katika kipute cha fainali ya Bongwe soka For Peace kati ya Bongwe United na Diani Stars ameelezea kuimarika kwa usalama katika eneo hilo baada ya kushuhudiwa kwa visa vya utovu wa usalama miezi michache iliyopita.
“ Sababu iliyotuleta hapa ilikuwa ni utovu wa nidhamu miongoni mwa vijana na taasubi kuwa eneo hili halina amani na usalama ,tumekuja kwa miezi mitatu na hatujashuhudia purukushani ya aina yeyote na ndio maana leo hii tunasherehekea ujio wa amani na usalama katika lokesheni hii ya Diani,” Asema bw.Mohamed.
Mwakilishi wa wanawake kaunti ya Kwale Fatuma Masito ameahidi kushirikiana na shirika la Sambasports Youth Agenda na shirikisho la FKF Kwale katika mchakato huo wakukuza talanta za vijana ili kuhakikisha kwamba wanajinasua katika jinamizi la utumizi wa mihadarati na visa vya utovu wa usalama.
Aidha ameelezea kuridhishwa kwake na jinsi akinadada walivyojitosa katika fani ya soko ,akiitaja kama njiamojawapo ya kuepuka dhulma za kijinsia katika jamii .
Ngarambe hio ya fainali ya siku ya jumapili katika uwanja wa Shamu , timu ya Bongwe United iliibuka na ushindi wa bao mbili dhidi ya Diani Stars waliopata bao moja.


Comments
Post a Comment