WASHUKIWA 26 WA UHALIFU WAKAMATWA DIANI.

Maafisa wa usalama Msambweni 

Taarifa yake : Caroline Katana

Washukiwa 26 wa uhalifu waliokuwa wamejihami kwa mapanga wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Diani kaunti ya Kwale baada ya kukamatwa katika oparesheni ya pamoja iliyofanywa na asasi za usalama eneo la Msambweni usiku wa Jumanne.

Vijana hao wenye kati ya umri wa miaka 14 hadi 21 wanadaiwa kuwahangaisha wenyeji kwa kuwakatakata mapanga kabla ya kuwaibia mali zao.

Washukiwa hao ambao ni miongoni mwa magenge ya wahalifu yanayosakwa na polisi wamekamatwa katika eneo la Kibundani ,Kona ya Musa ,Ibiza na Bongwe.

Mwenyekiti wa kamati ya usalama ambae pia ni naibu kamishna eneo la Msambweni Josphat Mutisya amesema kuwa washukiwa hao walikwepa mkono wa sheria siku ya Jumapili baada ya kuwajeruhi wakaazi muda mfupi baada ya kukamilika kwa mchezo wa soka katika uwanja wa Shamu.

“ Maafisa wa polisi walipata hizo habari wakafika katika eneo la tukio lakini hawakufaulu kuwakamata ,mikakati ya msako wa pamoja iliafikiwa na usiku wa Jumanne tukafaulu kuwakamata washukiwa hawa ishirini na sita ambao wanahatarisha usalama wa wenyeji na wageni katika eneo hili la Msambweni ,”Asema bw.Mutisya.

Naibu kamishna Msambweni Josphat Mutisya 

Mji wa kibiashara wa Diani na Ukunda umekuwa ukishuhudia misururu ya visa vya uhalifu jambo ambalo idara ya usalama imesema kuwa haitolivumilia.

“ Tungependa kuelezea wenyeji na wageni kwamba usalama umeimarishwa , asasi za usalama ziko tayari kukabiliana na magenge hayo ,huu msako unaendelea hadi tuhakikishe washukiwa wote wako chini ya sheria ,” Asema bw. Mutisya.

Afisa huyo wa usalama amelitaja swala la utumizi wa dawa za kulevya , vijana kukosa kujishughulisha na shughuli za maendeleo kuwa changizo kuu ya vijana kujiingiza katika maswala ya uhalifu.







“Ni sharti vijana watafute mwafaka wa kujiendeleza kimaisha kwa njia zilizo halali, kuketi maskani na kutumia mihadarati kisha badae kutekeleza visa vya uhalifu kama vyombo vya usalama hatutalikubali,” Asisitiza bw.Mutisya.

Kamishna huyo amewataka wazazi kuzingatia ulezi wa watoto wao kikamilifu ili wapate haki msingi ya elimu.

“ Watoto wakipata elimu bora nafasi ya kujiingiza kwa visa vya uhalifu huwa finyu sana ,wakipata msingi bora wa maisha huishi maisha ya uadilifu katika siku za usoni ,” Asema bw.Mutisya.

Mkasa huo wa Jumapili umeacha mkaazi mmoja akiuguza majeraha ya panga hospitalini baada ya kushambuliwa na magenge hayo ya uhalifu japo yuko katika hali nzuri .

Comments

Popular posts from this blog

Kwale Doctors Strike Enters Day 3 Amid Chaos, Unpaid Salaries, and Deteriorating Healthcare Services

Lack of focus on sanitation and hygiene interventions puts children at risk of death due to bacterial infections causing diarrhea in Kilifi County.

CHAMA CHA UZALENDO CHA TISHIA KUJIONDOA KATIKA MUUNGANO WA AZIMIO