KAUNTI YA KWALE KUJIUNGA NA KESI YA ARDHI YA MBUGUNI
Serikali ya Kaunti ya Kwale imetangaza kuwa itajiunga kama mdau katika kesi inayoendelea mahakamani kuhusu umiliki wa ardhi ya Mpango wa Makazi wa Mbuguni, Wadi ya Tsimba Golini, Kaunti Ndogo ya Matuga, ili kutetea haki za wakazi wanaopinga utoaji unaodaiwa kuwa kinyume cha sheria wa hati miliki. Hatua hiyo imetangazwa na Gavana Fatuma Achani baada ya wakazi kulalamikia kile walichodai kuwa baadhi ya hati miliki zilitolewa kwa watu wasiokuwa wenyeji wa eneo hilo pamoja na watu wenye ushawishi, hali iliyozua hofu ya kupokonywa ardhi wanayoitegemea kwa makazi na shughuli za kujipatia riziki. Mpango wa Makazi wa Mbuguni una takriban vipande 756 vya ardhi vilivyo katika vijiji vya Bang'a, Mteza, Mrera, Mbuguni na Lunguma. Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mbuguni kujadili mzozo huo, Gavana Achani alisema serikali yake haitavumilia unyakuzi wa ardhi na imejizatiti kushirikiana na timu ya mawakili wa wakazi kuhakikisha haki inatendeka. "Serika...