Misitu ya Kwale Hatarini: Mashirika Yaunganisha Nguvu Kupambana na Mabadiliko ya Tabia Nchi
![]() |
| Wanaharakati wa kukabiliana na mazingira. |
Na Jumwa
Mabadiliko ya tabia nchi yameendelea kutajwa kama changamoto kubwa inayochangia kuharibika kwa mazingira, hali inayowasukuma wanaharakati na mashirika ya kijamii kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
Katika Kaunti ya Kwale, gatuzi za Matuga, Msambweni na Kinango ni miongoni mwa maeneo yanayoshuhudia juhudi hizo kupitia mashirika saba ya kijamii yaliyoungana kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira.
Hatua hiyo inajiri wakati ambapo shughuli za ukataji miti kiholela zimeelezwa kuongezeka kwa kasi, hali inayochangia kupungua kwa misitu katika baadhi ya maeneo ya pwani.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa shirika la Tulinde Future Yetu Initiative, , mradi wao umejikita zaidi katika uhifadhi wa misitu kutokana na umuhimu wake kwa mazingira na sekta ya utalii.
“Tumejikita zaidi katika kuhamasisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira kupitia uhifadhi wa misitu. Ukataji wa miti umepelekea kupotea kwa baadhi ya ndege ambao wamekuwa kivutio cha utalii, hivyo tunataka kurejesha asili iliyokuwemo katika misitu yetu,” alisema Chiguza.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Imara chini ya mwamvuli wa Sikiliza Sauti Dunia Inaita, uliodhaminiwa na WeWorld, Chiguza alisema mashirika saba yameungana kwa lengo la kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha, alisema kuwa kampeni hiyo itatumia mbinu ya midahalo mashuleni ili kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira tangu wakiwa wadogo.
“Tumechagua kuwajumuisha wanafunzi katika midahalo kwani itawasaidia kufahamu umuhimu wa kuhifadhi mazingira wakiwa bado wachanga. Hawa ndio watakaokuwa mabalozi wa mazingira katika maisha yao ya baadaye,” aliongeza Chiguza.
Kwa upande wake, Katibu wa Kaya Kaunti ya Kwale, , amepongeza juhudi hizo akisema misitu imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya jamii za pwani.
Randani alieleza kuwa misitu imekuwa ikitumika kama chanzo cha dawa za asili pamoja na maeneo ya ibada, hivyo kuna haja ya kuhakikisha inalindwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
“Misitu imekuwa ikitumika kama dawa, na mti wa mbuyu uko katika hatari ya kutoweka. Zamani tulikuwa tukitumia maeneo hayo kama sehemu za kuabudu, hivyo ni muhimu kuyaifadhi na kueneza ujumbe huu kwa vizazi vichanga,” alisema Randani.
Naye afisa wa WeWorld, , alisema mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi minane katika kaunti za Kwale, Isiolo na Nairobi kwa lengo la kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
John alisema Kaunti ya Kwale imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili zikiwemo bahari na misitu, hivyo ni jukumu la mashirika na jamii kuhakikisha rasilimali hizo zinahifadhiwa.
“Kupitia miradi hii, baadhi ya makundi yatajikita katika uhifadhi wa rasilimali za bahari kama mikoko ili viumbe vinavyotegemea mazingira hayo viendelee kuwa salama,” alisema John.



Comments
Post a Comment