VIJANA KWALE WALAUMIWA KUPUUZA VIKAO VYA MAONI, WATAHADHARISHWA KUPITWA NA MAENDELEO

 ‎

Na Mwandishi Wetu Jumwa Kwale

Wito umetolewa kwa vijana katika kaunti ya Kwale kujitokeza kwa wingi kushiriki vikao vya maoni vinavyoandaliwa katika maeneo yao, huku ikielezwa kuwa wengi wao wameendelea kubaki nyuma kimaendeleo kutokana na tabia ya kutohudhuria mikutano hiyo muhimu ya kijamii na kiutawala.

Imeelezwa kuwa kupitia vikao hivyo, wananchi hupata nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu miradi na maendeleo wanayotaka kuona katika maeneo yao, lakini vijana wengi wamekuwa wakikosa kushiriki licha ya kuwa wao ndio nguvu kazi ya taifa.

Changamoto hiyo imewafanya wanaharakati na mashirika ya kijamii kuanza kutafuta mbinu mpya zitakazowavutia vijana kuhudhuria vikao vya maoni kwa hiari yao bila kusubiri mialiko rasmi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa INUA-IG katika kaunti ya Kwale, Mwenyekiti wa shirika la Tulinde Future Yetu Initiative, alisema mradi huo unalenga kuwaelimisha vijana, kina mama na watu wanaoishi na ulemavu kuhusu masuala ya utawala bora, uwajibikaji wa jamii na utetezi wa haki za binadamu kupitia mafunzo ya kidigitali.

“Tumejikita katika kuwaelimisha vijana, kina mama na watu wanaoishi na ulemavu kuhusu utawala bora kupitia mafunzo ya kidigitali, uwajibikaji kwa jamii na utetezi wa haki za binadamu,” alisema Chidzuga.

Mradi huo unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia mashirika ya META Consortium, FEMNET na WECF International unatarajiwa kuwapa vijana nafasi zaidi ya kujijenga kiuwezo kupitia mafunzo mbalimbali ya kijamii na kidigitali.

Kwa mujibu wa Chidzuga, zaidi ya vijana 1,000 wanatarajiwa kufaidika moja kwa moja na mradi huo huku wanawake zaidi ya 400 pamoja na watu 88 wanaoishi na ulemavu wakinufaika kupitia mafunzo na kampeni za uhamasishaji zinazotarajiwa kufanyika kupitia redio na njia nyingine za mawasiliano.

Kwa upande wake, mwakilishi wa vijana katika masuala ya utawala, amepongeza uzinduzi wa mradi huo akisema kuwa utasaidia kuwawezesha wanawake wengi kufahamu haki zao na kushiriki kikamilifu katika masuala ya maendeleo.

“Katika mradi huu wamegusia Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa nambari tano kuhusu usawa wa kijinsia. Kina mama wengi hawana ufahamu kuhusu haki zao, hivyo wakielimishwa jamii nzima itanufaika,” alisema Anzazi.

Aidha alisema mafunzo ya kidigitali yatasaidia wananchi wa mashinani kushiriki mijadala ya maendeleo kupitia simu zao na kuongeza ushiriki wao katika masuala ya utawala.

Naye mwakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu, alisema mradi huo ni fursa muhimu kwa kundi hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiachwa nyuma katika mipango ya maendeleo.

“Mara nyingi sisi watu wanaoishi na ulemavu tumekuwa tukisahaulika. Kupitia mradi huu tumepewa sauti ya kueleza changamoto tunazopitia na kushiriki kikamilifu katika jamii,” alisema Mwema.

Kwa upande mwingine, Afisa wa Vijana wa gatuzi la Msambweni na Lungalunga, aliwataka vijana kutumia vyema fursa hiyo ya mafunzo ya kidigitali hasa kipindi hiki ambacho taifa linaelekea katika mazingira ya kisiasa kuelekea uchaguzi.

“Mradi huu umekuja wakati mwafaka. Vijana wanapaswa kutumia mafunzo haya kufanya maamuzi sahihi kwa njia za kidigitali na kuepuka matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii,” alisema Gidhinji.

Mashirika ya kijamii sasa yana matumaini kuwa kupitia mafunzo hayo, vijana wengi wa Kwale wataanza kushiriki kikamilifu katika vikao vya maoni na michakato ya maendeleo ili kuhakikisha sauti zao zinasikika katika jamii.

Comments

Popular posts from this blog

Where Waste Becomes a Livelihood

Kwale Women Seek Bigger Voice in Coastal Fisheries and Blue Economy.

Kenya Power Celebrates Customer Service Gains as Kwale Customer Base Hits 106,000.