KAMPENI ZAPAMBA MOTO KABLA YA UCHAGUZI WA CHAMA CHA WAFANYAKAZI WA BANDARINI
MWANAHABARI: SHOKAH JUMA
Kampeni za uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Bandarini (DWU) zimeanza kushika kasi huku wanachama wakijiandaa kwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Agosti 13 mwaka huu.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Abubakar Mohammed Abdullahi, ameanza rasmi kampeni zake na kwa sasa ndiye mgombea pekee ambaye ametangaza nia ya kuwania wadhifa wa Katibu Mkuu, nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kubatilishwa kwa uchaguzi wa awali.
Abubakar amekuwa akifanya mikutano katika maeneo mbalimbali ya makazi ya wafanyakazi wa bandarini akiwashawishi wanachama kumpigia kura siku ya uchaguzi.
Katiba ya DWU inaeleza kuwa anayewania nafasi ya Katibu Mkuu lazima awe mtu wa nje ya ajira ya chama, huku mfanyakazi yeyote anayenuia kugombea akitakiwa kujiuzulu kazi kwa kutoa notisi kwa mwajiri wake.
Jitihada za kupata maoni kutoka kwa Suliman Otieno Owuor na Salim Kumaka hazikufanikiwa baada ya simu zetu kutopokelewa.
Abubakar ni miongoni mwa maafisa wa chama waliowahi kufutwa kazi katika Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) pamoja na viongozi wengine wa chama kufuatia mgomo uliotangazwa kuwa haramu wakati wa uongozi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa KPA marehemu Francis Gichiri Ndua.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Kazi na Mahusiano Kazini (ELRC) iliyoko Mombasa, ambapo Jaji Ocharo Kebira alibatilisha uchaguzi uliomweka Suliman Otieno Owuor kuwa Katibu Mkuu wa chama.
Mahakama ilielekeza DWU kufanya uchaguzi mpya ndani ya siku 60 kwa kuzingatia kikamilifu katiba ya chama pamoja na sheria husika.
Katika uamuzi wake, Jaji Kebira alisema uchaguzi uliofanyika mwezi Aprili ulikuwa batili baada ya kubainika kuwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi alipokea malalamiko mbalimbali kuhusu mchakato huo lakini akaendelea kuwasajili viongozi waliodaiwa kuchaguliwa.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kitaifa wa DWU, Mohammed Mwasera, ametangaza rasmi kuwa uchaguzi huo utafanyika Agosti 13, akiwataka wanachama zaidi ya elfu tano kushiriki kwa amani, nidhamu na kuheshimu misingi ya demokrasia pamoja na utawala wa sheria.
Comments
Post a Comment