Kilimo Himilivu Chabadilisha Maisha ya Wakulima Kinango
Na Jumwa Mwandoro
Kwa miaka mingi, eneo la Kinango, Kaunti ya Kwale, limekuwa likitajwa kama mojawapo ya maeneo yanayokumbwa na ukame wa mara kwa mara, hali iliyosababisha uhaba wa chakula na changamoto za kiuchumi kwa wakazi wake. Hata hivyo, juhudi za Shirika la Climate Care zinaanza kubadilisha taswira hiyo kupitia miradi ya kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Kupitia mradi wa "Sikiliza Sauti, Dunia Inaita", unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Shirika la WeWorld, Climate Care linafundisha zaidi ya makundi 20 ya wanawake na vijana yameanza kunufaika na mafunzo yanayolenga kuboresha mbinu za kilimo na kuimarisha usalama wa chakula.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Climate Care, Peter Tsuma, alisema lengo kuu la mradi huo ni kuwajengea wakulima uwezo wa kutumia mbinu za kisasa na rafiki kwa mazingira ili kuongeza uzalishaji wa mazao licha ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
"Makundi haya 20 yatakuwa mabalozi wa kuwafikia wakulima wengine katika jamii. Tunataka wakulima waachane na utegemezi wa zao moja, hususan mahindi, na badala yake walime mazao mbalimbali yanayoweza kustahimili ukame. Mafunzo haya yatawawezesha kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao," alisema Tsuma.
Alieleza kuwa wakulima wanafundishwa mbinu za kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua ili kuhakikisha mazao yanapata unyevu wa kutosha hata wakati wa kiangazi.
Tsuma pia alisema mradi huo unahamasisha matumizi ya mbinu za kilimo cha asili ili kupunguza utegemezi wa kemikali ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.
"Tunatumia mbinu za asili kupunguza gharama za uzalishaji. Kwa mfano, tunatumia mkojo wa sungura kutengeneza dawa ya kuua wadudu na mimea ya kienyeji kama kivumbani kutengeneza viuatilifu vya asili. Hii imeboresha uzalishaji huku tukilinda afya ya walaji na mazingira," aliongeza.
Kwa upande wake, Naibu Chifu wa eneo hilo, Vitalis Bodwe Moma, aliusifu mradi huo akisema unawapa wanawake na vijana maarifa muhimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia kilimo himilivu.
Aliwahimiza wanufaika kutumia kikamilifu mafunzo wanayopata ili kujiajiri, kuongeza kipato na kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira katika eneo hilo.
"Mafunzo haya yanatoa fursa kwa vijana na wanawake kujitegemea kiuchumi. Nawasihi wayachukulie kwa uzito ili yawe chachu ya maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla," alisema Moma.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Lucy Kisilu, alisema mafunzo hayo yamewasaidia kupata mbegu bora na ujuzi wa kuzalisha mazao kwa kutumia mbinu za kilimo hai, jambo ambalo limeongeza mavuno na kuboresha lishe za familia zao.
Aliongeza kuwa matumizi ya mbinu za asili yamechangia kuboresha afya za watoto wao, huku ufugaji wa kuku nao ukiimarika kutokana na elimu waliyoipata kuhusu utunzaji wa mifugo na upatikanaji wa masoko.
"Leo tunapata mazao bora, afya za watoto wetu zimeimarika, na hata ufugaji wetu wa kuku umeongezeka. Pia sasa tuna soko la uhakika la kuuza mifugo na mazao yetu, jambo ambalo limeongeza kipato cha familia zetu," alisema Kisilu.
Mradi wa "Sikiliza Sauti, Dunia Inaita" unatarajiwa kuongeza uwezo wa jamii za Kinango kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia kilimo endelevu, matumizi bora ya rasilimali za maji na mbinu za uzalishaji zinazolinda mazingira.
Comments
Post a Comment