Serikali ya Kwale yarejesha barabara ya umma ya kuingia ufukweni Diani
Na Shokah Juma
Serikali ya Kaunti ya Kwale kwa ushirikiano na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imerejesha eneo la umma la ekari 1.14 lililotengwa kwa ajili ya barabara ya kuingia ufukweni katika eneo la Diani, Kaunti Ndogo ya Msambweni, lenye thamani ya takriban Sh45 milioni.
Eneo hilo lilikuwa limenyakuliwa na kampuni binafsi kwa zaidi ya miongo mitatu, hali iliyowazuia wananchi, wavuvi na wafanyabiashara wa ufukweni kutumia njia hiyo kufikia Bahari ya Hindi.
Kurejeshwa kwa ardhi hiyo kunafuatia uamuzi wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Kwale uliotolewa Julai 14, 2026, uliobatilisha mkataba wa upangishaji wa miaka 99 uliotolewa mwaka 1994 pamoja na cheti cha umiliki, na kuagiza eneo hilo lirejeshwe kuwa mali ya umma.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa rasmi kwa eneo hilo, Gavana wa Kwale Fatuma Achani alisema hatua hiyo ni ushindi dhidi ya unyakuzi wa ardhi na itasaidia kurejesha haki kwa wananchi waliokosa fursa ya kutumia mali ya umma kwa miaka mingi.
Alisema serikali ya kaunti itaendelea kushirikiana na EACC kuhakikisha ardhi yote ya umma iliyonyakuliwa inafuatiliwa na kurejeshwa kwa manufaa ya wananchi.
Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Abdi Ahmed Mohamud, alisema tume hiyo itaendelea kufuatilia na kurejesha mali nyingine za umma zilizopatikana kwa njia isiyo halali, akisisitiza kuwa jukumu lao ni kulinda rasilimali za umma.
Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Ufukwe wa Diani (BMU), Ali Mwatsetse, alisema kurejeshwa kwa njia hiyo kutarahisisha shughuli za uvuvi, utalii na biashara zinazotegemea ufukwe.
Hii ni mara ya nne katika kipindi cha hivi karibuni ambapo Serikali ya Kaunti ya Kwale imefanikiwa kurejesha ardhi ya umma, baada ya kurejesha ekari 31 katika Kisiwa cha Chale, ardhi katika Kisiwa cha Kisite Mpunguti na ekari 13 katika Diani zenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mbunge wa Msambweni Feisal Bader, Mbunge wa Lunga Lunga Mangale Chiforomodo, Mwanasheria wa Kaunti Salim Gombeni, Waziri wa Ardhi Saumu Beja, MCA wa Mwereni Manza Beja, MCA wa kuteuliwa Eliza Mjeni pamoja na viongozi wengine wa kaunti na wananchi.
Comments
Post a Comment