FAYAZ BAKERS YAAGA SISI NI DOLA CUP, AZAM FC YATINGA NUSU FAINALI
Mabingwa watetezi wa michuano ya SISI NI DOLA Cup, Fayaz Bakers, wameaga mashindano hayo baada ya kutandikwa mabao 2-1 na Azam FC katika mchezo wa robo fainali uliochezwa katika uwanja wa Mombasa Sports Club.
Azam FC walionyesha ubabe mapema katika kipindi cha kwanza, wakifungua ukurasa wa mabao kupitia Harith Mshamanga dakika ya 20, kabla ya Ali Cheusi kuongeza la pili dakika ya 28 na kuifanya Azam FC kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa mabao 2-0.
Fayaz Bakers walirejea kipindi cha pili wakiwa na matumaini ya kubadili matokeo, na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 52 baada ya Rashid Nzao kufunga bao la kufutia machozi.
Hata hivyo, Fayaz Bakers walishindwa kupata bao la kusawazisha hadi dakika 90 zilipotimia, na hivyo Azam FC kutinga hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa mabao 2-1.
Azam FC sasa watavaana na Al Shifaa katika hatua ya nusu fainali, huku wakisaka tiketi ya kuingia katika mchezo wa fainali wa michuano hiyo.
Nyota wa mchezo huo, Hassan Kizianda wa Azam FC, amesema ushindi huo haukupatikana kwa urahisi, bali ulitokana na kujituma kwa wachezaji.
Amesema kikosi hicho kitaendelea kuboresha kiwango chake ili kufikia azma ya kutwaa ubingwa wa SISI NI DOLA Cup.
Kwa upande wake, Kocha wa Azam FC, Mshee Mohamed, amesema wachezaji wake walitekeleza vyema maelekezo ya benchi la ufundi na kutumia nafasi walizopata, jambo lililowasaidia kupata ushindi.
Kocha huyo amewataka vijana kujikita katika michezo, hususan soka, na kujiepusha na vitendo visivyofaa katika jamii.
Mmoja wa waandaaji wa michuano hiyo, Faruk Feisal, amesema SISI NI DOLA Cup imeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa vijana kuonyesha vipaji vyao, huku baadhi yao tayari wakipata fursa za kujiunga na timu zinazoshiriki katika madaraja ya juu.
Amesisitiza umuhimu wa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuendelea kuwaunga mkono vijana na kukuza vipaji vya soka katika ukanda wa Pwani.
Michuano hiyo inaendelea leo kwa mchezo wa kwanza wa nusu fainali kati ya Nyundo FC na Green Eagles, mchezo unaotarajiwa kuanza majira ya alasiri.
Comments
Post a Comment