MOMBASA SPORTS CLUB NA AL SHIFAA ZATINGA ROBO FAINALI KWA KISHINDO, SISI NI DOLA CUP YAPAMBA MOTO


Michuano ya SISI NI DOLA CUP imeendelea kushika kasi huku timu mbalimbali zikionyesha ushindani wa hali ya juu katika hatua ya 16 bora, na baadhi yao kufanikiwa kujikatia tiketi ya robo fainali.

Green Eagles ilikuwa timu ya kwanza kufuzu robo fainali baada ya kuichapa Mtwapa All Stars bao 1-0, lililofungwa na Paul Otieno katika dakika ya 59.

Likoni United nayo ilisonga mbele baada ya kuibwaga Goodhope kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za kawaida. Sasa Likoni United itakutana na Green Eagles katika robo fainali.

Nyundo FC iliendeleza ubabe wake kwa kuichapa Simba Apparel mabao 3-0. Swaleh Juma alifunga bao moja huku Joshi Ndela akiongeza mawili na kuipeleka timu hiyo hatua inayofuata.

Mombasa Sports Club ilifuzu kwa kishindo baada ya kuifunga Mombasa Kings mabao 3-1. Salim Ali aliiongoza timu yake kwa kufunga mabao mawili, huku Solomon Wanguzi akiongeza bao la tatu. Bao pekee la Mombasa Kings lilifungwa na Ali Tauz. Salim Ali alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi.

Al Shifaa nayo ilijikatia tiketi ya robo fainali kwa kuichapa Fetuwe FC mabao 2-1. Shariff Majabe aliifungia Al Shifaa bao moja huku bao lingine likitokana na kujifunga kwa Juma Mwinyi wa Fetuwe. Bao la Fetuwe lilifungwa na Laban Otieno. Abdulrahman Mwinyi alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi.

Katika robo fainali, Al Shifaa itakutana na Mombasa Sports Club katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Mechi nyingine za hatua ya 16 bora zitawakutanisha Azam United dhidi ya Wananyuki FC na Fayaz Bakers dhidi ya Kombani Youth, huku washindi wakitarajiwa kukutana hatua inayofuata.

Makocha wa timu zinazoshiriki michuano hiyo wamepongeza kiwango cha ushindani na vipaji vinavyoonyeshwa na vijana, wakitoa wito kwa timu za Ligi Kuu kuwafuatilia na kuwapa nafasi ya kucheza soka la kiwango cha juu.

Waandalizi wa SISI NI DOLA CUP wamewahimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi viwanjani kuendelea kuwapa hamasa vijana hao wanapoendelea kupigania ubingwa.

Comments

Popular posts from this blog

Where Waste Becomes a Livelihood

Kwale Women Seek Bigger Voice in Coastal Fisheries and Blue Economy.

Kenya Power Celebrates Customer Service Gains as Kwale Customer Base Hits 106,000.