MZEE MOHAMED ACHANI AZIKWA KWA HESHIMA, VIONGOZI NA MAELFU YA WANANCHI WAMUAGA
Na Shoka Juma
BODO, KWALE — Viongozi wa kitaifa na kaunti, pamoja na maelfu ya wananchi, wamejitokeza kutoa heshima za mwisho kwa Mzee Mohamed Achani, baba mzazi wa Gavana wa Kaunti ya Kwale, Fatuma Achani, aliyezikwa nyumbani kwake katika kijiji cha Bodo, wadi ya Ramisi, kaunti ndogo ya Msambweni.
Mzee Achani, mwenye umri wa miaka 80, alifariki Jumatatu asubuhi, Oktoba 19, 2026, baada ya kupata matatizo ya kiafya alipokuwa akitekeleza swala ya Alfajiri.
Akizungumza kwa niaba ya Rais William Ruto wakati wa mazishi hayo, Waziri wa Michezo, Vijana na Uchumi wa Ubunifu, Salim Mvurya, aliwasilisha salamu za rambirambi za Rais kwa Gavana Fatuma Achani, familia yake na wananchi wa Kwale kufuatia msiba huo.
Mvurya aliwataka Wakenya kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, huku akiwakosoa wanasiasa wanaochochea ukabila na migawanyiko nchini kuelekea uchaguzi ujao.
Alisema Wakenya wanapaswa kuwakataa wanasiasa wanaotumia ukabila kuwagawa wananchi, akimtaja Rais Ruto kama kiongozi anayepaswa kuungwa mkono katika juhudi za kuimarisha umoja wa kitaifa.
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Kwale, Chirema Kombo, alitoa shukrani kwa viongozi wa kitaifa na kaunti, majirani, marafiki na wananchi waliojitokeza kuifariji familia ya Gavana Achani katika kipindi hicho kigumu.
Kombo alisema serikali ya kaunti imethamini msaada wa kihisia na kimwili uliotolewa kwa gavana na familia yake wakati wa maombolezo ya kumpoteza baba yao.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Nassir, Naibu Gavana wa Kilifi, Florence Chibule, Mbunge wa Likoni, Mishi Mboko, Mwakilishi wa Wanawake wa Kwale, Fatuma Masito, na Spika wa Bunge la Kaunti ya Kwale, Seth Kamanza.
Aidha, wabunge wa Kwale, Feisal Badar wa Msambweni, Mangale Chiforomodo wa Lunga Lunga, Gonzi Rai wa Kinango na Kassim Tandaza wa Matuga, walijiunga na viongozi wengine kutoa rambirambi zao kwa familia ya marehemu.
Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na wajumbe wa Bunge la Kaunti ya Kwale, mawaziri wa kaunti (CECs), maafisa wakuu wa serikali, wakurugenzi, viongozi wa dini na viongozi wa jamii, ambao waliungana na familia ya Achani katika kumuaga mpendwa wao.
Comments
Post a Comment