ZAIDI YA MICHE 100,000 YA MIKOKO YAPANDWA KWALE KATIKA JUHUDI ZA KUHIFADHI MAZINGIRA


Na Hafsa Juma

Serikali ya Kaunti ya Kwale, mashirika yasiyo ya kiserikali na wakazi wa Mwamdudu, katika eneo bunge la Samburu, wameungana kupanda zaidi ya miche 100,000 ya mikoko katika juhudi za kuhifadhi mazingira ya baharini na kuimarisha shughuli za kiuchumi zinazotegemea rasilimali za bahari.

Zoezi hilo lililenga kuhamasisha ushirikiano kati ya jamii, mashirika na serikali katika kulinda mifumo ikolojia ya baharini, huku wakazi wakihimizwa kutumia fursa zinazotokana na uhifadhi wa mazingira kuboresha maisha yao kiuchumi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Elvis Katana kutoka shirika la Furaha na Baraka Farm alisema shirika hilo linaendelea kuwawezesha wakazi wanaoishi karibu na misitu ya mikoko kujipatia kipato kupitia shughuli zinazohusiana na uhifadhi wa mazingira, zikiwemo ufugaji wa nyuki na ukuzaji wa samaki.

Alisema lengo ni kuhakikisha kuwa juhudi za kuhifadhi mazingira zinaenda sambamba na kuboresha maisha ya jamii zinazotegemea rasilimali hizo.

“Jukumu letu kuu kama mashirika yasiyo ya kiserikali ni kusaidia kuhifadhi mazingira na kuhakikisha kuwa jamii zinazoishi karibu na misitu zinanufaika kiuchumi. Tunawawezesha kufanya shughuli kama ufugaji wa nyuki na ufugaji wa samaki ili kuboresha maisha yao,” alisema Katana.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Kwale, David Rotich, aliwapongeza wakazi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo, akisema upanzi wa mikoko ni sehemu ya juhudi pana za kitaifa za kuongeza idadi ya miti nchini.

Rotich alisema Kaunti ya Kwale imepiga hatua katika juhudi za upanzi wa miti, akifichua kuwa miche zaidi ya milioni 14 imepandwa ndani ya miezi sita iliyopita.

“Ningependa kuwafahamisha kuwa ndani ya miezi sita, Kaunti ya Kwale imepanda zaidi ya miche milioni 14. Nimefurahishwa sana na jinsi wakazi walivyojitokeza kwa wingi na kufanikisha zoezi hili,” alisema Rotich.

Naye Waziri wa Mazingira wa Kaunti ya Kwale, Saumu Beja, aliwataka wakazi kuhakikisha miche yote iliyopandwa inalindwa na kutunzwa hadi ikomae, akisisitiza kuwa upanzi wa miti pekee hautoshi bila utunzaji wa muda mrefu.

Alisema jamii zinapaswa kubadilisha mtazamo kutoka kupanda miti na kuzingatia pia kuikuza ili kuhakikisha inatimiza malengo ya uhifadhi wa mazingira.

“Kauli mbiu yetu si kupanda tu, bali ni kukuza. Kupanda ni jambo linaloweza kuchukua dakika tano, lakini kukuza mti kunahitaji muda na juhudi. Ningependa kusisitiza kuwa Jumuiya za Misitu (CFAs) zinapaswa kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa,” alisema Beja.

Beja aliongeza kuwa serikali ya kaunti ina mpango wa kuanzisha mradi wa usimamizi wa vyanzo vya maji kwa ushirikiano na jumuiya za misitu, unaotarajiwa kugharimu shilingi milioni 150.

Alisema mradi huo utalenga kuimarisha ushirikiano na jumuiya hizo katika usimamizi wa mazingira na kuendeleza shughuli zinazoweza kuboresha maisha ya wakazi.

Aidha, Mwakilishi wa Wadi ya Kasemeni, Victor Safar Nyanje, alizitaka mashirika zaidi kujitokeza kusaidia jamii kupata miche ya kutosha ya mikoko na rasilimali za kifedha zitakazowawezesha kuendeleza juhudi za uhifadhi.

Alisema wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika shughuli za upanzi na utunzaji wa mikoko, hivyo wanahitaji kuungwa mkono ili kuendeleza juhudi hizo na kuimarisha maisha yao kiuchumi.
“Ningeomba mashirika yalete miche ya kutosha kwa wanawake hawa na pia kutoa fedha zitakazowawezesha kujikimu kiuchumi, kwa sababu wanawake wameonyesha bidii kubwa katika jamii,” alisema Nyanje.

Mikoko ina mchango mkubwa katika kulinda maeneo ya pwani dhidi ya mmomonyoko wa udongo, kutoa makazi na mazalia kwa viumbe wa baharini, pamoja na kuimarisha shughuli za uvuvi ambazo ni chanzo muhimu cha mapato kwa jamii za pwani.

Aidha, misitu hiyo husaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kufyonza na kuhifadhi hewa ukaa, hivyo kuifanya kuwa rasilimali muhimu katika juhudi za kukabiliana na changamoto za kimazingira.

Zoezi hilo ni sehemu ya juhudi pana za uhifadhi wa mazingira nchini Kenya, ambayo imeweka lengo la kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032.

Hata hivyo, mafanikio ya juhudi hizo hayatategemea idadi ya miche inayopandwa pekee, bali pia uwezo wa jamii na wadau kuhakikisha miti hiyo inatunzwa hadi ikue na kutimiza jukumu lake la kulinda mazingira na kuimarisha maisha ya wananchi.

Comments

Popular posts from this blog

Where Waste Becomes a Livelihood

Kwale Women Seek Bigger Voice in Coastal Fisheries and Blue Economy.

Kenya Power Celebrates Customer Service Gains as Kwale Customer Base Hits 106,000.